Thursday, May 30, 2019

Ndoa ya Lulu Sintofahamu

Ndoa ya Lulu Sintofahamu

Moja ya ndoa za mastaa Bongo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa ni ya msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’ lakini sasa hali ya sintofahamu imegubika, Amani limebaini.

Sintofahamu hiyo inakuja kufuatia ukimya uliotawala kwani tangu mchumba wa staa huyo, Francis Siza ‘Majizo’ amvishe pete mwishoni mwa mwaka jana, hakujawa na chochote kilichoendelea huku wahusika wakiwa wamekausha.

Awali ilidaiwa kuwa, baada ya tukio la Lulu kuvishwa pete, taratibu za ndoa zilikuwa zikifanyika kimyakimya na kwamba ingefanyika bonge la sherehe lakini cha kushangaza wahusika wanaendelea na maisha yao mengine.

Wakizungumza na Amani kwa nyakati tofauti, baadhi ya wadau walisema kuwa, wanatamani kuona tukio hilo la kihistoria linafanyika kwani wamechoka kusubiri. “Miongoni mwa mashabiki kindakindaki wa Lulu mimi ni mmoja wao, nilifurahi sana kuona amevishwa pete, sasa nashangaa hii sintofahamu,” alisema Subira Kessy wa Kinondoni jijini Dar.

Naye Mama Janeth ambaye hakujitambulisha anatoka wapi aliandika kupitia ukurasa wa Instagram baada ya kuona picha mpya za Lulu:

“Waooo…umependeza sana mama, natamani useme hapo ilikuwa kwenye kitchen party yako. Kwani nini tatizo mama, au umeshafunga ndoa kimyakimya? Tuambie tujue maana hii sintofahamu inatutesa.”

Mbali na wadau hao walioonesha kutojua chochote kinachoendelea kuhusu ndoa ya staa huyo, wapo ambao walieleza kuwa, yawezekana imeshafungwa kimyakimya ili kuepusha manenomaneno. “Kuna kipindi Lulu na Majizo walienda China, isije ikawa walienda kule na kumaliza kila kitu. Maana masuala ya kufunga ndoa kwa mbwembwe ni uamuzi wa mtu, sijui lakini…,” alisema Juma Kiloi wa Mwenge, Dar.

MAKONDA ALIWAHI KUSEMA

Katika kukoleza sintofahamu, hata Mkuu wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye aliwahi kueleza kuwa atakuwa mwenyekiti wa kamati ya harusi ya mastaa hao, miezi kadhaa nyuma aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram hivi: “…heri Majizo ameamua kufungia China, sasa tunasubiri send-off huku (Bongo)…”

TUJIKUMBUSHE

Lulu na Majizo wamekuwa pamoja kwa muda mrefu kabla ya mwezi Septemba mwaka jana kuingia kwenye uchumba rasmi ambapo Makonda aliwahi kusema kuwa, atahakikisha wawili hao wanaingia kwenye maisha ya ndoa haraka. Baada ya tukio la kuvishana pete, wachumba wao walisafiri kwenda China, huko ikadaiwa walifunga ndoa simpo lakini taarifa hizo hazikuwahi kuthibitishwa.

Baadaye zikavuja taarifa kuwa, ndoa ya wawili hao inasukwa chinichini na itafanyika bonge la pati bila watu kuchangishwa lakini mpaka leo kimya kimetawala. Gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta Lulu kupitia simu yake ya mkononi lakini kila ilipopigwa iliita bila kupokelewa. Simu ya Majizo haikuwa hewani, hata hivyo jitihada za kuwatafuta zinaendelea.

No comments:

Post a Comment