Wednesday, July 3, 2019

Mke wa Mtawala wa Dubai Akimbilia Mafichoni

Mke wa Mtawala wa Dubai Akimbilia Mafichoni

Mke wa mtawala wa Dubai Sheikh Mohammed Al Maktoum , Binti Mfalme Haya Bint al-Hussein, yuko mafichoni jijini London akidaiwa kuhofia usalama wa maisha yake baada ya kumtoroka mumewe.


Sheikh Mohammed, 69, ambaye ni bilionea, aliandika utenzi wenye hisia za hasira kwenye ukurasa wa Instagram akimshutumu mwanamke ambaye hakufahamika kwa vitendo vya ”udanganyifu na usaliti”.

Mke wa kiongozi huyo mzaliwa wa Jordan 45, aliolewa na Sheikh Mohammed mwaka 2004 na kuwa mke wa sita, ”mke mdogo”.

Sheikh Mohammed ameripotiwa kuwa na watoto 23 kutoka kwa wake zake.

Binti mfalme Haya awali alitorokea Ujerumani mwaka huu kutafuta hifadhi. Hivi sasa anaelezwa kuishi kwenye nyumba ya thamani ya pauni milioni 85 Kensington Palace Gardens, katikati mwa jiji la London, akijiandaa kufungua mashtaka kwenye mahakama ya juu.

Je ni nini kilichomfanya ayakimbie maisha yake ya anasa huko Dubai na kwanini anasema kuwa ”anahofu kuhusu maisha yake”?

Vyanzo vya karibu naye vinasema Bibi Haya hivi karibuni alibaini ukweli ambao ulimshitua kuhusu kurejea kwa Sheikha Latifa Dubai mwaka jana, mmoja wa mabinti wa mtawala huyo.Alitoroka Jumuia ya falme za kiarabu kwa njia ya bahari akisaidiwa na mwanaume mmoja mfaransa lakini alinaswa na watu wenye silaha kwenye pwani ya India na akarudishwa Dubai.

Bibi Haya, pamoja na rais wa zamani wa Ireland Mary Robinson , walikingia kifua hadhi ya Dubai kuhusu tukio hilo.

Mamlaka za Dubai zimesema binti Sheikha Latifa alikuwa akipitia vitendo vya ”unyanyasaji” na ”alikuwa salama Dubai”.Lakini mawakili watetezi wa haki za binaadamu walisema alichukuliwa kwa nguvu .

Tangu wakati huo inadaiwa kuwa Bibi Haya alijua ukweli kuhusu tukio hilo na kwa sababu hiyo hakuwa na mahusiano mazuri na familia ya mumewe na alikuwa akifanyiwa visa mpaka alipoona kuwa hayuko salama tena.

Chanzo kilicho karibu naye kimesema ana hofu kuwa na yeye atachukuliwa kwa nguvu na ”kurejeshwa” Dubai. Ubalozi wa Jumuia ya falme za kiarabu jijini London umekataa kutoa kauli yoyote kuhusu suala hilo walilosema kuwa ni masuala binafsi baina ya watu hao wawili.Binti Mfalme Haya kiwa kwenye picha ya pamoja na Mwanamfalme Charles na mkewe Camilla

Hatahivyo, kuna masuala ya uhusiano wa kimataifa kwenye suala hili.

Binti mfalme Haya, ambaye alipata elimu yake nchini Uingereza, na kusoma chuo cha Oxford nchini humo anafikiriwa kuwa anataka kuishi Uingereza.

Ikiwa mumewe atataka kurudishwa kwa mkewe, suala hili litakuwa na mvutano wa kidiplomasia kwa Uingereza, ambayo ni mshirika wa karibu wa jumuia ya falme za kiarabu.

Suala hili pia litaiweka njia panda Jordan kwa kuwa Bibi Haya ni Dada wa mfalme wa Jordan Abdullah. Karibu robo milioni ya raia wa Jordan wanafanya kazi jumuia ya falme za kiarabu, na Jordan haiwezi kuingia uhasama na Dubai.

No comments:

Post a Comment